ULANGA
Na Fatuma Mtemangani
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.dtk.John Pombe Magufuli alisema kuwa fedha za Serikali ya Awamu ya Tano hazitaliwa kwa urahisi hivyo amewaonya makandarasi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maji ambao wamechukua fedha na kushindwa kukamilisha kazi zao na kutoweka, watakuwa wamekula sumu, tena sumu kali.
Hata hivyo amesema kwamba wafadhili wa nchi mbalimbali zikiwemo za Umoja wa Ulaya (EU), Marekani pamoja na Uingereza wanaendelea kutoa ufadhili wa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kutokana na kuaminiwa katika kusimamia vyema matumizi ya fedha za maendeleo ya wananchi pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi.
Mh.Rais Magufuli aliyasema hayo katika ziara yake ya kikazi katika eneo la Nyandeo, Kata ya Kidatu wilayani Kilombero mkoani Morogoro, wakati wa kuweka jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kidatu- Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 inayojumuisha ujenzi wa daraja la mto Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 130.
Alisema kutokana na kutumia vyema fedha za umma ndiyo maana Serikali ya Tanzania inaaminika na kumedhihirishwa kutokana EU, Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DIFD/Ukaid) na Shirika la Maendeleo la Kimataifa ya Marakani (USAID), kuwezesha ufadhili wa fedha kiasi cha asilimia 49.15 (Uingereza asilimia 40.13 na Usaid 10.72) katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara.
“Nashukuru wafadhili mbalimbali bado wanaipenda Tanzania kwa kusaidia kutoa fedha za maendeleo ikiwemo ya barabara Kidatu- Ifakara na nawataka wananchi kutoa ushirikiano wa kuwa walinzi na mali za serikali,” alisema Rais Magufuli.
Pia mh.rais Aliwataka makandarasi wa barabara hiyo, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wakala wa Barabara (Tanroads), kuikamilisha kwa wakati na ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa wa Aprili 2, 2020 kwa kuwa tayari fedha zipo za mradi huo, huku akiwataka wananchi wa maeneo hayo waitunze bara bara hiyo kwa manufaa yao na Taifa.
Aidha, aliwaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi kupitia miradi yote ya maji ili kujua miradi ambayo haijatekelezwa na kutokamilika wakati fedha zimetolewa kwa makandarasi hao warudi kumalizia, kurejesha fedha na wakiwa wametoweka, watafutwe mahali popote walipo ili wakamatwe.
Hivyo aliagiza Takukuru, Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuwatafuta na wafikishwe mahakamani kwa kutumia sheria ya Bodi ya Makandarasi inayotaja kifungo cha miaka minne au mitano jela na kurudisha fedha.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema ujenzi wa barabara ya Kidatu- Ifakara unafanywa na Kampuni ya Renolds Construction Company Ltd yenye makao yake makuu nchini Nigeria na pia mradi wa ujenzi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo wa Nchi za Ulaya (EDF) ukishirikiana na UKaid na Usaid.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa kujumisha malipo ya fidia, misamaha ya kodi, tozo mbalimbali na uhamishaji wa miundombinu ya umeme na maji na utagharimu kiasi cha Sh bilioni 104.914. Alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutaunganisha eneo muhimu la Ukuzaji na Uzalishaji wa Kilimo la Ukanda wa Kusini (SAGCOT) na kuwa kiungo muhimu cha barabara kuu ya Tanzam kuanzia Mikumi – Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Londo hadi Lumecha (Songea) na barabara ya kutoka Ifakara – Mahenge.
Alisema barabara hiyo itasaidia kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao na malighafi kutoka na kwenda katika bonde la Mto Kilombero hususani wilaya za Kilosa, Kilombero, Ulanga, Malinyi na maeneo mengine ya Mkoa wa Morogoro na nchi kwa ujumla.
Naye Mwakilishi wa DFID nchini, Beth Arthy alisema Serikali ya Uingereza kupitia mashirika yake yataendelea kutoa misaada ya ufadhili wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kutambua umuhimu wake katika kuendeleza ukuaji wa uchumi wa wananchi na Taifa la Tanzania,pia Balozi wa EU nchini Tanzania, Roeland Van De Geer alisema umoja huo kwa kushirikiana na mashirika mengine ya nchi mbalimbali yapo tayari kuunga mkono kusaidia maendeleo ya Tanzania.
Rais Magufili yuko mkoani Morogoro katika ziara yake ya kikazi na katika ziara hii Mh.Rais ameweka jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kidatu- Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9,ufunguzi wa daraja la mto kilombero lenye urefu wa mita mia tatu themanini na nne{384}ambalo pia linajumuisho na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara unganishi zenye urefu wa kilometa tisa nukta mia moja na arobaini na mbili{ 9.14}2, ambalo ni miongoni mwa madaja makubwa sabini na saba likiwa na mita 384 huku daraja la Mkapa likishika nafasi ya kwanza kwa ukubwa likiwa na mita mia tisa sabini nukta tano{970.5}.
MWISHO.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.