Watumishi Wilayani Ulanga Mkoani Morogoro wametakiwa kutimiza wajibu wao wawapo kazini ili kutoa huduma stahiki na kwa wakati kwa wananchi wanaowahudumia.
Akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Ulanga wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bwana Clifford Tandari amesema kuwa watumishi wote wanapaswa kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi kwa wakati kwani ni sehemu ya kutimiza majukumu yao.
Ameongeza kuwa watumishi hao wanapaswa kufanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu za kazi zao ikiwa ni pamoja na kufika kazini kwa wakati yaani saa moja na nusu asubuhi hadi saa tisa na nusu jioni na kuvaa vitambulisho vya kazi ili wananchi wamtambue anayewapatia huduma kinyume na hapo ni kuwanyima fursa wananchi kupata huduma.
Aidha amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bwana Yusuf Sumuguruka kuwatawanya watumishi katika maeneo yenye upungufu wa watumishi walioondolewa kwa kukosa vyeti ikiwemo zahanati na shule ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kupata huduma wakati mkoa ukisubiria kupata kibari cha ajira.
Hata hivyo amewasihi watumishi kuwa wavumilivu wakati serikali ikishughulikia suala la ulipaji wa madeni yao na wakati ukifika wote watalipwa hivyo kwasasa wafanye kazi kwa umoja na mshikamo ili kuleta maendeleo ya wilaya na wananchi.
Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi Juni 23 ambapo kwa wilaya ya Ulanga imedhimisha kwa kuongeza muda wa saa moja kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi.
Mwandishi: Sekela Mwasubila
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.