Na Yuster Sengo
Halmashauri ya wilaya ya ulanga mkoani morogoro imetenga shilingi milioni tisini na sita na laki nane kwa ajili ya kuvikopesha vikundi zaidi ya arobaini vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vilivyopo katika tarafa za Lupiro,Vigoi,Mwaya na Ruaha wilayani hapa.
Akithibitisha hilo afisa maendeleo ya jamii wilayani hapa Bwana Mohamed Atiki amesema wilaya ya ulanga inatekeleza sheria inayotaka kila halmashauri itenge asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili kuyawezesha makundi hayo kujiinua kiuchumi na kufikia malengo.
‘’Katika utekelezaji huu wa sheria halmashauri imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inatoa mikopo hiyo kwa mujibu wa sheria,kwa maana katika utekelezaji wa bajeti yetu katika mwaka huu tunaoendelea nao halmashauri imeweza kutenga jumla ya shilingi milioni 96.8 kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya wajasiliamali wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu’’alisema Bwana Atiki.
Aidha Bwana Atiki amesema kuwa katika kuhakikisha vikundi vyote 48 vitakavyopatiwa mikopo katika mwaka huu wa fedha ofisi yake ya maendeleo ya jamii inaendesha mafunzo kwa vikundi vyote ili viweze kutambua matumizi sahihi ya fedha na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mikopo hiyo ambayo inatolewa bila riba inalenga kuviwezesha vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi na zenye tija ili viweze kutimiza azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.
‘’Leo hii kama unavyotuona ndio tupo katika mafunzo tukianzia tarafa ambayo inajumla ya vikundi 11 kwa ajili ya kuviwezesha mkopo huo na baada ya vigoi tunatarajia kwenda tarafa za lupiro na mwaya’’ alisema Atiki
‘’Faida walizonazo hawa wanavikundi fedha hizi hazina riba kwaiyo ni fedha ambazo tunategemea zitakwenda kuwasaidia vizuri katika uendelezaji wa biashara zao’’ alisema Atiki.
kwa upande wake Bi Sigrinda Mdemu ambaye pia ni afisa kutoka ofisi ya maendeleo ya jamii wilayani hapa amewataka wanavikundi hao kuzitumia fedha walizoomba kwa malengo ili waweze kuzirudisha na kuiwezesha halmashauri kukopesha vikundi vingine kwa mwaka wa fedha unaofuata.
tayari vikundi kutoka tarafa ya Lupiro na Vigoi vimepatiwa mafunzo na fedha zao tayari zimeingia kwenye akaunti huku vikundi vya tarafa ya Mwaya vikitakiwa kujiandaa na zoezi hilo.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.