ULANGA
Na
Fatuma Mtemangani
Mradi wa kinga dhidi ya maambukizi ya VVU na athari za UKIMWI kwa Wasichana balehe na Wanawake Vijana kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Maendeleo ya Jamii) umezinduliwa Wilayani Ulanga mkoani Morogoro na mkuu wa wilaya ya Ulanga ndugu Jackob Joseph Kassema.
Mradi huo una lengo la kutoa mafunzo ya malezi na makuzi kwa wasichana balehe na wanawake vijana walioko shule na nje ya mfumo wa elimu,kutoa elimu ya ujasiriamali na stadi za maisha kwa walio nje ya mfumo wa elimu,kuwapatia pedi wasichana walioko shule na nje ya mfumo wa elimu,kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU kwa mikoa mitatu ikiwemo mkoa wa Dodoma,Singida na Morogoro.
Akizungumzia mafanikio yatakayo patikana ndani ya mradi huo kaimu mkurugenzi wa mradi huo bwana Mapunda amesema kua kwa mkoa wa morogoro mradi huo utatekelezwa katika wilaya ya Ulanga,Malinyi pamoja na Ifakara DC kwa kutoa elimu waelimishaji rika,wazazi wa wasichana balehe,kujikinga na maambukizi ya VVU ikiwemo upigaji wa simu na ujumbe mfupi bure ili kupata taarifa muhimu na usahihi.
Hata hivyo bwana Mapunda amesema kuwa Mradi utatekelezwa katika kata na vijiji vyote ambavyo vimefikiwa na mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini katika Halmashauri za Malinyi, Ulanga na Ifakara.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga ndugu Jackob Kassema ameshukuru mradi wa kinga dhidi ya maambukizi ya VVU na athari za UKIMWI kwa Wasichana balehe na Wanawake Vijana katika Wilaya ya Ulanga kwani Wilaya ya Ulanga ni Wilaya inayofanya vizuri kupitia miradi mbalimbali wanayopata.
Hivyo mkuu wa Wilaya ndug Kassema amewataka waanzilishi wa miradi hiyo kuwa endelevu ili iweze kusaidia kwa vizazi vya sasa na baadae kwani wananchi walio wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya maambukizi ya VVU na athari za UKIMWI kwa Wasichana balehe na Wanawake Vijana
“ Nawasihi wananchi wangu Hatari ya Maambukizi ya VVU kwa Wasichana Balehe na Wanawake Vijana hivyo kama mzazi au mlezi jenga tamaduni ya kuzungumza na motto wako wa kike ili asiingie kwenye vishawishi kabla ya umri wake kufikia na kukatisha ndoto zake”.
Hatari ya Maambukizi ya VVU kwa Wasichana Balehe na Wanawake Vijana yanachangiwa na sababu kuu 3 ambazo ni sababu za kitabia (behavioral), za kibaiolojia (biological) na mtambuka (structural),Umaskini wa kipato katika kaya unawaweka Wasichana Balehe na Wanawake Vijana katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU kwa kushiriki ngono zisizo salama ili kupata kipato na Wasichana waliokatisha masomo hawapati mbinu mbadala za kujikimu kimaisha zikiwemo stadi za maisha na ujasiriamali hivyo kuwa kwenye hatari ya kushiriki biashara ya ngono ambayo ni kichocheo kikubwa cha maambukizi ya VVU
Aidha Kutokana na kufanya ngono zisizo salama, kundi hili lipo kwenye hatari ya kupata mimba za utotoni, kuolewa katika umri mdogo na kufanyiwa vitendo vingine vya ukatili vinavyochangia uwezekano wa kupata maambukizi ya VVU.
Kutokana na changamoto hizo,Serikali kupitia usaidizi wa GF, imeamua kuanzisha na kuendeleza mpango wa VVU na UKIMWI kwa kundi la Wasichana Balehe na Wanawake Vijana ikiwemo Kubadili tabia,mpango wa upimaji wa VVU na matibabu ya UKIMWI,Afya ya Uzazi,kuondoa umaskini wa kipato na mtambuka.
Katika kupunguza umaskini wa kipato, mradi huu utalenga kaya maskini zaidi kama zitakavyokuwa zikiainishwa na mpango wa kunusuru kaya maskini inayoratibiwa na TASAF, kwa kutumia mfumo wa utoaji wa ruzuku kwa kaya maskini zaidi.
“Katika utekelezaji wa mpango huu, ni jukumu la Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha kwamba miradi ya aina hii inaoanishwa na majukumu ya msingi ya kada ya Maendeleo ya Jamii ya kuelimisha, kuhamasisha na kuikinga jamii dhidi ya athari zinazotokana na harakati za kujitafutia maendeleo”.
Mwisho.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.